
Wanahabari wapewa mafunzo kuripoti uhalifu wa mazingira

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyotolewa kwa wanahabari 20 kutoka vyombo vya habari tofauti.
Akizungmza wakati wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana , Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Yonas Alfred ameeleza mazingira ni rasilimali muhimu kwa jamii na Taifa.
Amesema waandishi wanapaswa kuandika habari za kuisaidia serikali na kuleta maendeleo kwa sababu suala la mazingira ni uhai na maisha ya kila mwananchi hivyo kupitia habari jamii itatambua umuhimu wa mazingira ili vizazi vijavyo viendelee kunufaika na rasilimali hiyo.
” Muandike habari za uchokonozi kwenye uhalifu wa masuala ya uhifadhi wa mazingira mfano katika maeneo ya Kanda ya Ziwa yanakabiliwa na uvuvi haramu, uharibifu wa maliasili,ukataji miti na uchomaji wa mkaa pasipo kufuata taratibu hivyo jamii itakapopata elimu itasaidia kuyanusuru mazingira na kuwa na matumizi mbadala ” amesema
Naye Mratibu wa OJADACT, Lucyphine kilanga amesema kuwa mafunzo hayo ya kuwajengea uelewa waandishi yatakuwa chachu ya kuleta mabadiliko ndani ya jamii na uelewa wa kutambua umuhimu wa kuyatunza hivyo waandishi wanapaswa kuandika habari bora zaidi za uhalifu wa mazingira.
Mwenyekiti wa OJADACT, Edwin Soko amesema kuwa suala la uhalifu ni jinai hivyo Aprili 9 mwaka huu watendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wengine wa Tanzania Bara ili kukuza wigo la wao kuandika habari za uchunguzi hasa za uhalifu katika nyanja mbalimbali ikiwemo uhalifu wa misitu.